Jumatatu , 3rd Apr , 2017

Jumuiya ya Ulaya (EU) imeipatia Tanzania msaada wa shilingi bilioni 490 kwa ajili ya kusaidia bajeti kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Majengo ya Benki Kuu ya Tanzania

Sehemu kubwa ya fedha hizo zimeelekezwa kwenye maboresho ya mfumo wa ukusanyaji mapato pamoja na sera zinazosimamia masuala ya utawala katika fedha.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Dotto James na Mwakilishi wa Jumuiya ya Ulaya hapa nchini Bw. Roeland Van De Geer ndiyo waliyosaini makubaliano ya utolewaji wa msada huo leo Jijini Dar es Salaam, ambapo kusainiwa kwake kunafanya jumla ya msaada wa kimaendeleo unaotolewa na Jumuiya hiyo kati ya mwaka 2014 na mwaka 2020 kufikia shilingi trilioni 1.5.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Bw. Dotto amesema kutolewa kwa fedha hizo kumetokana na Jumuiya ya Ulaya kuridhishwa na umakini wa serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hasa mageuzi ya kiuchumi kupitia ujenzi wa uchumi wa viwanda.