Ijumaa , 29th Oct , 2021

Serikali ya Ujerumani imeipatia Tanzania msaada mwingine wa Euro milioni 45 sawa na takribani shilingi za Tanzania bilioni 119.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu katika sekta za maji, afya na kuendeleza sekta ya maliasili na utalii.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Regine Hess

Akizungumza baada ya kusaini mikataba hiyo mipya mitatu kwa niaba ya Serikali, na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mheshimiwa Regine Hess kwa niaba ya Ujerumani, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, amesema kuwa fedha hizo zitaisaidia nchi kukabiliana na athari za Uviko 19, kuboresha uhifadhi wa mazingira na huduma za jamii.

Amesema kuwa mkataba wa kwanza uliosainiwa unahusisha mradi wa kuboresha upatikanaji wa maji na udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi na mradi wa kuboresha huduma za afya uliiotengewa kiasi cha Euro milioni 16.5 sawa shilingi bilioni 43.73.

"Katika fedha hizo kiasi cha Euro milioni 6 kitatumika kuboresha huduma ya maji kwenye miji ya Mbeya, Songwe na Tunduma ambapo zaidi ya watu 500,000 wanatarajiwa kunufaika na huduma hiyo pamoja na kutoa ajira ya watu 2,000 katika sekta ya maji kwenye maeneo hayo", amesema Katibu Mkuu

Aidha amefafanua zaidi kuwa mradi wa uboreshaji wa huduma ya afya umetengewa Euro milioni 10.5 na una lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika mikoa ya Tanga na Mbeya.

Tutuba amesema mradi mwingine unaofadhiliwa na Ujerumani una thamani ya Euro milioni 8.5 sawa na shilingi bilioni 22.53 zitakazotumika kwa ajili ya kufunga mitambo maalumu ya kidigitali itakayosaidia kudhibiti magari ya watalii yanayoingia kwenye Hifadhi za Taifa yasiharibu mazingira katika Hifadhi nne za Serengeti, Burigi-Chato, Katavi na Mikumi.

 "Mkataba wa tatu tuliosaini unahusisha msaada wa Euro milioni 20 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 53 zilizotolewa kama fedha za dharura kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa fedha uliotokana na athari za ugonjwa wa uviko 19 katika sekta ya maliasili na utalii". ameongeza Tutuba.