Jumapili , 27th Dec , 2020

Mwaka huu, hofu ilitanda nchini Tanzania baada ya kuripotiwa mtu wa kwanza kupata maambukizi ya virusi vya corona na ilizidi kufuatia kifo cha kwanza cha mgonjwa wa Covid-19, kutangazwa.

Watu wengi waliingia wasiwasi kutokana na ongezeko la takwimu za wagonjwa kutangazwa kila siku. Wengine walianza kujiandaa kwa kujifungia ndani (lockdown) ili kuepuka maambukizi na kusababisha shule zote, vikiwemo vyuo kufungwa Machi 17, kunusuru maisha ya watoto.

Rosemary Pawa ni mmoja wa watu waliojifungia kutokana na hofu ya corona. Anasema kuwa alijifungia ndani (lockdown) kwa miezi sita ili kuepuka maambukizi ya virusi vya hivyo.

“Nilikuwa na hofu kubwa kutokana na hali yangu ya kiafya kwani nina ugonjwa wa lupus (ni ugonjwa ambao kinga za mwili zinashambulia mwili badala ya kuukinga) na taarifa pia zilikuwa zinanitatiza kwani wanasema kuwa watu wenye kinga duni ni rahisi kupata virusi hivyo.”

“Wataalamu wa afya wanasema sisi wagonjwa wa lupus kinga zetu ziko chini hivyo nilikuwa na hofu kubwa kwamba hata nikitoka nje ya nyumba naweza kupata maambukizi halafu sitaweza kupona,”anaeleza Rosemary.

Deo Senya ambaye ni mfanyabiashara ndogo ndogo, eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, ni mmoja wa waathirika wa kuambukizwa virusi vya corona. Anasema kuwa aliambukizwa virusi hivyo na mteja aliyefika dukani kwakwe bila kuchukua tahadhari za kiafya.

“Nilianza kupata dalili na nikawa nahisi huenda ni corona, mimi nikajifukiza nikapata nafuu, lakini wakati nimepata virusi hivyo mke wangu alikuwa na ujauzito wa miezi tisa karibu ya kujifungua na yeye akapata virusi hivyo.”

“Kwa wakati huo nilihangaika sana kupata matibabu kwani hata hospitali nilizokuwa nikienda wahudumu wa afya walikuwa na hofu nilikataliwa hospitali sita, wote walikuwa na hofu ya kuambukizwa.”

“Lakini baadae nilikuja kufanikiwa nilipoenda hospitali moja wapo hapa Dar es Salaam na mke wangu alikuwa na hali mbaya sana kwa bahati nzuri alihudumiwa na akajifungua salama,”anaeleza Senya.

WALIVYOISHINDA HOFU

Maambukizi ya virusi vya corona hayajaripotiwi tena nchini. Hii ni baada ya watu waliokuwa karantini kupona na kuruhusiwa kutoka, huku kambi zote zilizowekwa kwa ajili ya karantini zikifungwa na maisha kurejea kama kawaida.

Rosemary aliyejifungia ndani kwa muda wa miezi sita, ametoka na maisha yake yamerudi kama yalivyokuwa awali.

“Nilipata ujasiri wa kutoka nje na kuendelea na shughuli zangu za uelimishaji wa jamii kuhusu lupus baada ya serikali kutangaza kuwa ugonjwa umepungua. Kutokusikia takwimu mpya na taarifa za kuogopa ziliniongezea ujasiri zaidi, lakini hata sasa naendelea kuzingatia tahadhari zilizoshauriwa na wataalamu wa afya kama kunawa mikono kwa maji tiririka, kutumia sanitizer, kuepuka mikusanyiko na kuvaa barakoa,”anaeleza.

Kwa upande wake Senya anasema kuwa mwanzo alikuwa na hofu kutokana na taarifa anazopata kila siku kuhusu madhara makubwa yanayosabaishwa na ugonjwa huo katika maeneo mengine.

“Matangazo na taarifa zilikuwa zinatia hofu sana baada ya kutokusikia taarifa za mtu kufa nikaanza kujiamini na nikaanza kuimarika sasa hivi sivai barakoa ila mikono nanawa kwa maji tiririka na sabuni.”

“Kwa sasa hata mtu akipiga chafya sina wasiwasi ile hofu ya mwanzo imeondoka na familia yangu wote wazima na hakuna mwenye hofu ya corona tena licha ya kupata matatizo,”anasema.

Anaeleza kuwa kwasasa anaendelea na biashara zake japo bado hali ya biashara kwa kwe haijawa nzuri kwa upande wa mauzo.

HOFU ILIVYOTHIBITIWA NCHINI

Dk. Frank Mkui ni Mratibu wa magonjwa ya afya ya akili katika Mkoa wa Dar es Salaam, anasema hofu inaweza kuwa ya ugonjwa wa afya ya akili au ya kawaida ambayo inaweza kukabiliwa.

“Kuna ugonjwa wa hofu unaitwa ‘enziet’  mtu anakuwa na hofu bila kuelewa ni kwanini anakuwa na hofu, lakini kuna hofu ambazo zinatengenezwa. Mfano na vyombo vya habari au mitandao ya kijamii kuhusu kitu fulani dunia nzima hivyo watu wanaogopa kama vile corona aina hii ya hofu imetengenezwa,” anaeleza Dk. Mkui.

Anasema wakati wa mlipuko wa virusi vya corona watu wengi walianza kuchukua tahadhari kwa umakini kutokana na hofu ya ugonjwa huo. Anasema kuwa kwa sasa Watanzania wameweza kushinda hali ya hofu kuhusu virusi vya corona baada ya kupata taarifa nzuri kutoka kwa serikali.

“Hii ni baada ya serikali kuwatoa wasiwasi kuwa waendelee na kazi na ugonjwa umepungua hiyo ikamaliza hofu kisaikolojia watu wanawaamini viongozi hivyo wakisema kitu huwa ni rahisi kufanya. Sisi tumeshinda ugonjwa baada ya kufuata tahadhari na watu wakajiamini na mtu yeyote unayemwamini akikwambia kitu unaweza kufuata tunamshukuru rais alivyosema na sasa tuko salama kabisa,” anabainisha Dk. Mkui.

HOFU NI NINI?

Msaikolojia Tiba, Isaack Lema, kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), anasema hofu ni hali ambayo binadamu ameumbiwa na ni silika ya maisha ambayo inasaidia mtu kutambua hatari.

Anasema mtu anapokutana na hatari mbele yake hofu ni kama kengele inayojulisha kuwa kuna hatari mbele. Mabadiliko ambayo yanaweza kutokea kwenye mwili wa binadamu ni kupumua kwa kasi, mapigo ya moyo kwenda mbio, kutokwa jasho, tumbo kunguruma na wakati mwingine kuishiwa nguvu.

Kwa mujibu wa Lema, hofu inapotokea inaweza kuwa hali ya kawaida au isiwe ya kawaida. Anasema hofu isiyo ya kawaida huwa inatokea wakati hakuna hatari yoyote, lakini mtu anapata hisia ya kuwepo hatari na wakati huo mabadiliko ya mwili yanatokea kumjulisha ya kwamba kuna hatari.

“Kwahiyo anapopitia vile wakati hakuna hatari tunasema ni hofu iliyopitiliza ambayo ndio dalili au kiashiria cha magonjwa ya wasiwasi kipengele cha hofu.”

“Sasa hii ina tofauti na hali za wasiwasi kuhusu mjadala uliopo katika akili ya mtu na unakuwa hasi ambao unajirudia rudia ambao unaambiwa itakuwaje nikiachishwa kazi au itakuwaje nikiambukizwa corona hii pia ni tofauti na hofu inayombatana na hatari,” anaeleza.

Anasema mtu anapokuwa na hofu kinga mwili pia zinashuka na kuwa rahisi kushambuliwa na magonjwa hivyo kujiamini pia kunasaidia.

HALI YA CORONA DUNIANI

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi sasa zaidi ya watu milioni 37.2  duniani wameambukizwa virusi hivyo huku vifo vikiwa ni milioni 1.07 na waliopona ni milioni 27.9. 

Marekani ndio inayoongoza kwa kuwa na maambukizi mengi zaidi ya watu milioni saba, vifo 218,867 na waliopona ni 5,067,698. Kwa Bara la Afrika nchi ya Afrika Kusini ndio inayoongoza kwa  kuwa na maambukizi 688,352, waliofariki 17,547 na waliopona ni 620,081. Nchini Tanzania maambukizi ya corona yalidhibitiwa ni watu 509 pekee walioripotiwa kuambukizwa huku vifo vikiwa 21 na waliopona 183.