Jumatatu , 18th Mar , 2024

Shirika la Viwango nchini Tanzania (TBS) limesema kwamba chakula cha msaada kilichoongezwa virutubishi kilichotolewa na Wizara ya Kilimo ya Marekani, kwa ajili ya baadhi ya shule za mkoa wa Dodoma kilifuata taratibu za uingizwaji wa chakula nchini na kilipofika kilifanyiwa ukaguzi

Chakula cha msaada

na uchunguzi wa kimaabara na kuthibitishwa kuwa ni salama kwa matumizi.

Taarifa ya TBS imekuja saa chache tu mara baada ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kuitaka taasisi inayofanya mradi wa kutoa misaada ya chakula ikiwemo mchele ulioongezewa virutubisho katika shule mbalimbali mkoani Dodoma, waiambie Marekani kwamba Tanzania kuna mchele na maharage kwahiyo zile fedha wanazowapa wakulima wa Marekani wawape wakulima wa Tanzania na virutubisho viongezwe hapa nchini wakati Watanzania wakiwa wanaona.

Aidha TBS wameongeza kuwa, utaratibu wa kuongeza virutubishi kwenye chakula (food fortification) unakubalika kitaalamu na hufanyika kwa lengo la kuboresha hali ya lishe kwa walaji.

"TBS itaendelea kusimamia kikamilifu jukumu la kuhakikisha kuwa chakula kinachoingia nchini kinakidhi vigezo vya usalama na ubora kwa mujibu wa matakwa ya viwango ili kuendelea kulinda afya za walaji," imeeleza taarifa ya TBS