Ijumaa , 31st Jan , 2020

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA, siku ya leo Januari 31, 2020 imezindua tuzo zake ziitwazo ICT Awards, zenye lengo la kuwatambua watoa huduma katika sekta ya habari, mawasiliano na teknolojia ambao wapo chini ya mamlaka hiyo.

Picha ya tuzo za TCRA na ICT

Sababu za kuandaa tuzo hizo za habari, mawasiliano na teknolojia "ICT" ambazo zitakuwa chini ya TCRA ni kutoa zawadi za ubora kupitia kwenye taaluma  hiyo ya soko la Tanzania, kutambua ulazima wa ubora, bidhaa na huduma, kutoa shukrani kwa wateja na kuzingatia umuhimu na ongezeko la watumiaji na uzalishaji.

Tuzo hizo zitakuwa na vipengele 15  vitakavyoshindaniwa ila baadhi yao ni mtandao bora wa mwaka, kampuni inayotoa huduma bora ya internet, kituo bora cha runinga "TV" ya kitaifa, kituo bora cha TV wilaya, kituo bora cha radio kitaifa, kituo bora cha radio kimkoa, radio bora ya kijamii ya mwaka, kituo cha TV bora mitandaoni "Online TV", radio bora ya mitandaoni na tovuti bora ya mwaka.

Watoa huduma wenye kibali cha TCRA wanapaswa kujaza fomu  za kuwasilisha kazi zao kupitia tovuti ya ICT kuanzia leo Januari 31 hadi Machi 15, 2020.

Kura zitaanza kupigwa kuanzia Aprili 1 hadi 30, 2020 na tuzo zitatolewa Mei 15, 2020, Mlimani City, Dar es Salaam.