Jumanne , 14th Mei , 2019

Zaidi ya shilingi milioni 800 zinatarajiwa kutumika katika zoezi la kuwafunga mikanda ya mawasiliano ya kijiographia (GPS) tembo ambao wanapatikana hifadhi ya jamii ya wanyamapori ya Makao na Pori la Akiba la Maswa.

Tembo akiwa amevishwa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla amezindua mpango huo katika eneo la Makao WMA ambalo limewekezwa kwa kampuni ya Mwiba Holding, moja ya kampuni zilizochini ya Taasisi ya Friedkin Conservation Fund (FCF).

Waziri Kigwangala amesema vifaa hivyo vya GPS vitawezesha tembo kufuatiliwa mienendo yao na kudhibitiwa matukio ya Tembo kuvamia mashamba na masuala ya ujangili.

"Mpango huu pia kutakuwa na uzio wa technolojia ya kielekroniki, ambao utawezesha kuonekana tembo ambao wanatoka maeneo ya hifadhi kabla ya kufanya madhara", amesema Dk. Kigwangalla.

Mtafiti wa Tawiri Dk. Emmanuel Masenga amesema hadi sasa tembo 95 wamefungwa mikanda ya GPS maeneo mbali mbali ya hifadhi nchini.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amesema mpango huo wa kuwafunga tembo GPS utasaidia kuondoa migogoro baina ya wa hifadhi na jamii.