Jumatano , 4th Nov , 2020

Mgombea urais wa Marekani kupitia chama cha Republican Trump ametishia kwamba, ataenda mahakama za juu zaidi kupinga matokeo ya uchaguzi hii ni baada ya kudai kuwa uchaguzi huo umegubikwa na udanganyifu.

Mgombea urais wa Marekani kupitia chama cha Republican, Donald Trump.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Trump ameandika kuwa kura zimeibiwa, huku akitangaza kuwa tayari ameshashinda katika uchaguzi huo licha ya kwamba hata zoezi la kuhesabu kura bado halijamalizika.

"Tuko juu lakini wanajaribu kuiba uchaguzi, hatutawaacha wafanye hivyo, kura haziwezi kupigwa baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika", ameandika Trump.

Aidha Trump ameongeza kuwa "Ukweli ni kwamba tumeshinda na uchaguzi umegubikwa na udanganyifu, hii ni aibu kwa nchi yetu, tutaenda Mahakama ya juu zaidi kupinga matokeo ya uchaguzi".

Mpaka sasa kwa mujibu wa mtandao wa Fox News, mpinzani wa Trump, Joe Biden wa chama cha Democratic ana kura 238, na Trump ana kura 213.