
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (Kulia), Kushoto ni Baadhi ya wananchi wakipiga kura kwenye uchaguzi 2020 (Picha kutoka mtandaoni)
Akizungumza mara baada ya kusikiliza taarifa ya uchaguzi uliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage ameipongeza NEC na viongozi wake kwa kusimamia na kuendesha vizuri uchaguzi wa mwaka jana.
"Hakuna shaka kwa yeyote aliyeshuhudia ama kushiriki kwenye uchaguzi atakubaliana nami ulifanyika vizuri sana tena kwa kiwango cha juu kabisa,” amesema Rais Samia.
Pia akizungumzia mapendekezo yaliyotolewa na NEC, Rais Samia amewaomba wadau wakae na kuyashughulikia mapendekezo hayo yaliyotolewa kuhusu uchaguzi.
"Wadau wakae na kuangalia mapendekezo yaliyotolewa ya kuunganisha sheria ili uchaguzi mkuu na uchaguzi wa serikali za mitaa kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Wadau waeleze na sisi serikali tutaangalia cha kufanya,” ameeleza Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ametoa shukrani kwa Watanzania walijitokeza kupiga kura na kujiandikisha sambamaba na vyama vya siasa na wagombea wote walioshiriki uchaguzi wa 2020 pamoja na Chama cha Mapinduzi CCM kwa kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi huo uliopita.
Akiwasilisha ripoti ya Uchaguzi Mwenyekiti wa NEC Jaji Rufaa (Mst), Semistocles Kaijage amewasilisha pendekezo la wagombea ubunge na udiwani wanaopita bila kupingwa katika chaguzi wapigiwe kura huku akisema kuwa uchaguzi wa 2020 ulizingatia maadili na taratibu zote.