Ijumaa , 24th Mei , 2019

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na watoto, Ummy Mwalimu amesema yeye ni miongoni mwa wazazi ambao wamekuwa wakiwakagua watoto wao mara kwa mara ili kujua kama wamefanyiwa vitendo vya ukatili.

Waziri Ummy ametoa kauli hiyo Bungeni wakati wa muendelezo wa vikao vya Bunge ambapo alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Rombo, Joseph Selasin ambaye alihoji juu ya wazazi kupewa elimu ya kuzungumza na watoto wao.

Akijibu swali hilo, Ummy Mwalimu amesema, "wazazi tutimize wajibu wetu kwa watoto, mimi namkagua binti yangu, lazima tuwakague hawa watoto wa miaka 3 walau muogeshe utajua anachangamoto gani, tukiwa bize kutafuta hela watoto wanaharibika, mtoto analawitiwa miezi 3 mzazi hajui."

"Mwananchi yeyote ambaye ana taarifa kuhusiana na ukatili wa mtoto apige simu 116 itapokelewa na taarifa inafika kwenye vyombo vya Serikali, na itafanyiwa kazi, tumeanzisha madawati ya jinsia kwenye Jeshi la Polisi yapo madawati zaidi ya 350." ameongeza Waziri Ummy.

Kwa sasa Bunge linaendelea jijini Dodoma ambapo mawaziri mbalimbali wameendelea kuwasilisha makadirio ya bajeti zao kwa mwaka wa fedha 2018/2019.