Alhamisi , 5th Dec , 2019

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Barnabas Mwakalukwa, amesema kuwa Mwandishi wa Habari wa Radio Kwizera, mkoani humo George Bahamu, anayedai kutekwa na kutelekezwa porini huenda alikuwa na mambo yake binafsi kwa sababu mtekaji hawezi kukuacha kienyeji tu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Barnabas Mwakalukwa.

Akizungumza na EATV &EA Radio Digital, leo Desemba 5, 2019, Mwakalukwa amesema kuwa mtu yeyote aliyetekwa hawezi kupiga simu yake mwenyewe na kutaja eneo alipo.

"Huyo wala hajatekwa alikuwa na mambo yake binafsi, mtu aliyetekwa hawezi kuongea kwa simu na akasema jamani nipo mahala fulani, kwahiyo nimemtuma OCD akamuangalie anaweza akawa na mambo yake ya ajabu, pengine mambo ya wanawake, mnapenda tui 'destroy' Tasnia yenu ya Habari, mtu anayetekwa hapigi simu na watu hawakuachi kienyeji tu" amesema RPC Mwakalukwa.

Inadaiwa kuwa Mwandishi huyo ametoweka jana jioni Desemba 4, 2019 na asubuhi ya Desemba 5 alijikuta ametupwa katikati ya Pori, lililopo maeneo ya Ipuli mkoani humo, ambapo pia Kamanda Mwakalukwa amemuagiza Afisa Upelelezi kufika eneo la tukio.