
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema hayo katika mjadala wake aliyoshiriki wa kuimarisha upatikanaji endelevu wa rasilimali fedha katika sekta ya afya ambapo alieleza mipango mbalimbali na changamoto ambazo Tanzania na nchi nyingi za kiafrika zinakabiliwa nazo katika kufikia mipango endelevu ya upatikaji wa rasimali fedha.
"Katika kukabiliana na changamoto ya rasilimali fedha Tanzania inakamilisha mchakato wa kuwa na bima moja ya Taifa ya Afya ambapo pia itaweka sharti kwa kila mtu kuwa na bima ya afya ili kuwezesha wananchi kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua", alisema Ummy.
Pamoja na hayo, Waziri Ummy amesema kwamba serikali ya Tanzania imeanzisha mikakati mbalimbali ya kuhakikisha fedha kidogo zilizopo zinatumika vizuri. Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa fedha kwa Vituo vya huduma kulingana na matokeo au utendaji wao (Result Based Financing) ambapo vituo vya tiba vilivyokuwa na hali mbaya (nyota sifuri) vinapewa fedha kuboresha huduma ambapo maboresho makubwa yameonekana katika vituo hivyo ndani ya kipindi kifupi.
Waziri Ummy Mwalimu anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano muhimu wa kimataifa wa kuondoa vikwazo katika kuokoa maisha ya mama na mtoto unaofanyika Mjini Addis - Ababa, Ethiopia uliyoanza jana na kumalizika leo ambapo mkutano huo ulifunguliwa na Mhe. Dkt. Mulatu Teshome Rais wa Jamhuri ya watu wa Ethiopia