Alhamisi , 16th Sep , 2021

Wakili Edson Kilatu amesema tangu mwaka 2001 baada ya Marekani kushambuliwa na Al Qaeda, dunia iliingia kwenye ajenda ya kupambana na ugaidi, ambapo Tanzania ilianzisha sheria mwaka 2002.

Wakili Edson Kilatu

Kilatu ameyasema hayo leo Septemba 16, 2021 kwenye kipindi cha Supa Breakfast kinachoruka East Africa Radio Jumatatu mpaka Ijumaa saa 12:00 hadi 4:00 asubuhi.

''Kwa mujibu wa sheria yetu ya ugaidi ya mwaka 2002 kifungu cha pili kinazungumzia sheria hii kwa upande wa Tanzania inatumika Bara pamoja na Zanzibar pia sheria hii inaruhusu hata makosa ambayo yamefanyika nje ya mipaka ya Tanzania,'' amesema Wakili Edson kilatu.

Aidha Wakili Edson ameongeza kuwa, ''Hivyo kwa mujibu wa sheria hii hata kama mtu amekamatwa nje ya mipaka ya Tanzania anaweza kufikishwa kwenye Mahakama kuu Tanzania au Mahakama kuu Zanzibar''.

Pia amesema kuwa ili mtu aweze kushitakiwa kwa kosa la ugaidi ni lazima Mkurugenzi wa Mashtaka aweze kuridhia mtu husika afunguliwe mashtaka na kuongeza kuwa kifungu cha nne cha sheria ya ugaidi ndio kina ainisha ni makosa gani au mambo gani yanaweza kupelekea kosa la ugaidi kwanza kufanya kitu chochote kinachoweza kupelekea hujuma au uharibifu kwa nchi ama shirika la kijamii.