Alhamisi , 20th Oct , 2016

Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto, UNICEF limesema kwa sasa lina uwezo wa kuokoa maisha ya mamilioni ya watoto ulimwenguni wanaofariki kutokana na magonjwa hatari ya kuambukiza kama dondakoo, pepopunda, kifaduro, homa ya ini aina ya B na mafua

Mtoto akipatiwa chanjo

Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi cha UNICEF, Bi Shannelle Hall, amesema uwezo huo unafanikishwa kutokana na ubia wa chanjo duniani GAVI na wadau wengine, ambao utaiwezesha UNICEF kupata chanjo moja pekee yenye kuzuia magonjwa hayo matano ijulikanayo kama Pentavalent, kwa senti 87 kwa chanjo, ambayo ni nusu ya bei inayolipwa sasa.

Amesema UNICEF itanunua dozi milioni 450 mwakani na kuzipeleka katika nchi 80, ili kuokoa maisha ya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano katika nchi masikini zaidi, ambao hufariki dunia kwa asilimia kubwa kutokana ukosefu wa ufadhili wa chanjo.

Bi Shannelle ameongeza kuwa ni mara ya kwanza kabisa katika historia kuna soko la chanjo za bei nafuu ambapo nchi zinazojifadhili na zinazofadhiliwa, zote zina fursa sawa, ambalo ni jambo muhimu katika upatikanaji wa chanjo.