Jumatano , 20th Mar , 2024

Siku chache baada ya EATV kuripoti tukio la binti wa miaka 11 kufanyiwa ukatili wa kubakwa Jijini Mwanza, mtoto mwingine wa kiume (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 16 mkazi wa Buguku, Mkolani Jijini humo anadaiwa kulawitiwa.

Mtoto wa kiume (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 16 mkazi wa Buguku ambaye amelawitiwa

Mama mzazi wa mtoto huyo amesema tukio hilo lilitokea tangu tarehe 18 mwezi wa pili, lakini hadi sasa hakuna aliyechukuliwa hatua na Jeshi la Polisi huku akitakiwa kuwatafuta watuhumiwa mwenyewe.

"Maelezo yapo alichukuliwa katika kituo cha polisi Buhongwa na mpelelezi wa kesi hiyo ni wa pale kituo cha polisi Igogo, lakini nilishangaa aliponambia nenda nyumbani ila uwatafute hao watuhumiwa ukishawapata tu utupigie simu sisi tutakuja kuwakamata". Amesema mama huyo.

Baadhi ya majirani wameiambia EATV kuwa wamesikitishwa na ushirikiano mdogo walioupata kutoka kwa viongozi wao likiwemo jeshi la polisi, katika ufatilizi wa tukio hilo.

Naye kaimu Kamanda wa Polisi Mwanza Gideon Msuya,  akijibu malalamiko hayo kwa njia ya simu amesema ipo sheria inayoliongoza jeshi hilo hushirikiana na wananchi katika kuwasaka wahalifu.