Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amesema kuwa, katika kuhakikisha vijana wanajengewa uzoefu, serikali imedhamini vijana takribani 5000 katika mafunzo ya ufundi yatakayowawezesha kukidhi vigezo vya kuajiriwa na kupata ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kwa kujiajiri au kuajiri wenzao.
Aidha ameongeza kuwa serikali kupitia wizara ya elimu imesaini mkataba wa ushirikiano pamoja na wamiliki wa viwanda na taasisi binafsi ili kuwawezesha wanafunzi na wanavyuo kupata nafasi ya kufanya mazoezi kwa vitendo kwenye makampuni na taasisi hizo.
Amesema hatua hizo zitaondoa changamoto na kasumba ya vijana kuulizwa kuhusu uzoefu wao wa kazi, pindi watakapokuwa wanatafuta ajira katika taasisi binafsi.
Ameyasema hayo leo Februari 19, 2026 wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Vijana (Vijana Platform) Mkoani Mwanza.





