Jumamosi , 25th Mei , 2019

Mbunge wa Kilwa Kusini Suleiman Bungara maarufu kama 'Bwege', ameeleza kuwa alishikiliwa na polisi kwa muda kufuatia kutoa kauli ambayo imeonekana kupishana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi, kuhusiana na suala la vitambulisho vya mjasiriamali mdogo.

Bwege ambaye ni Mbunge wa Kilwa Kusini amesema kilichomponza ni hatua yake ya kuwataka wavuvi wasinunue vitambulisho, kwa kile alichokidai kuwa inatokana na wao kutokuwepo kwenye kundi la wajasiriamali wadogo.

"Ni kweli nilikamatwa tatizo ni suala la vitambulisho vya ujasiriamali mimi na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, hoja yangu ilikuwa wavuvi si wajasiriamali kwa sababu yeye anakata leseni ya uvuvi na haruhusiwi kwenda baharini, lakini mjasiriamali ni mfanyabiashara mdogomdogo lakini RC aliwataka wavuvi wanunue vitambulisho mimi niliwaambia walipe 23,000 tu ya leseni." amesema Mbunge Bwege.

"Nikashangaa nikipigiwa simu na OCD wa Kilwa kuwa nimepingana na kauli ya RC kuwa nimetoa kauli ya kichochezi na walinichukua wakaniweka ndani lakini baadaye walinitoa kwa dhamana." amesema Mbunge Bwege.

Disemba 10, 2018 Rais Magufuli alingilia kati sakata la kutotambuliwa kwa wafanyabiashara wadogo nchini kwa kuchapisha vitambulisho maalum kwaajili ya kuwatambua wafanyabiashara hao ili waweze kufanya kazi zao kwa uhuru na kuvikabidhi kwa wakuu wa mikoa.