Wakulima wakiuza mazao yao kupitia vyama vya ushirika
Wito huo umetolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini Bw. Tito Haule katika Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Warajis Wasaidizi Wa Vyama Vya Ushirika Wa Mikoa kilichofanyika leo mjini Dodoma Novemba 15, 2016.
“Sekta ya Ushirika ina mchango mkubwa katika kuwezesha kutimia kwa azma ya Serikali ya kukuza uchumi, hivyo kila mmoja wetu katika eneo lake tuweke msukumo katika vyama vya ushirika ili viweze kuwa sehemu ya utekelezaji wa azma hii ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuipeleka nchi yetu katika uchumi wa viwanda ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza kasi ya kufikia lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025,” alisema Mrajis.
Viwanda vinavyomaanishwa siyo lazima viwe viwanda vyenye kuhitaji mitambo mikubwa bali vinaweza kuanzishwa viwanda vidogovidogo ambavyo vitawezesha uchakataji wa mazao.
Bw. Haule akizungumzia kuhusu majukumu yatakayopewa kipaumbele na Tume ya Maendeleo ya Ushirika alisema ni kusimamia na kudhibiti badala ya kuwa wasuluhishi wa migogoro katika Vyama vya Ushirika.



