
Vyuo hivyo ni pamoja na chuo cha sayansi ya Kilimo na Teknolojia pamoja na Chuo cha Teknolojia ya Habari.
Hatua hiyo inakuja baada ya Vyuo hivyo Vishiriki vya Chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph chenye Kampasi nyingine jijini Arusha, Boko na Luguruni Dar es salaam kuwa na mlolongo wa matatizo ya ubora, uongozi, ukiukwaji wa sheria na taratibu za uendeshaji wa chuo kikuu .
Akiongea leo jijini Dar es salaam, Katibu Mtendaji wa TCU Prof.Yunus Mgaya amesema wanafunzi 2,046 wanaosoma katika ngazi ya Shahada katika vitivo mbalimbali vya vyuo hivyo watahamishiwa katika vyuo vikuu vingine kwa gharama za chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph pamoja na kuhamishwa kwenda vyuo vikuu vingine vinavyofundisha masomo yanayofananana masomo wanayosoma hivi sasa.
Prof. Mgaya amesema kufuatia uamuzi huo, wanafunzi wote wanaosoma katika vyuo vikuu hivyo vishiriki wanatakiwa kuondoka katika vyuo hivyo mara moja baada ya kukamilisha taratibu za kukabidhi mali na vifaa vingine vya vyuo hivyo na kutakiwa kuripoti kwenye vyuo watakavyopangiwa wakati wa kufunguliwa kwa muhula.
Prof. Mgaya ameongeza kuwa wanafunzi wote waliohamishwa ambao hawakukamilisha mitihani yao ya mwisho wa muhula wa kwanza na wengine ambao hawakukamilisha kabisa mitihani yao watatakiwa kukamilisha katika vyuo watakavyohamishiwa kwa utaratibu maalum.