Ijumaa , 8th Nov , 2019

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimepata fursa ya kutoa elimu ya uwekezaji  kwa Waheshimiwa/Wajumbe wa Kamati mbili za Bunge, kupitia semina iliyoendeshwa Novemba 7, Dodoma na kufunguliwa na Mhe. Angellah Kairuki WOM (Uwekezaji) na kuhudhuriwa na  Mwenyekiti wa Bodi ya TIC Prof. Longnus

Pichani ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Geoffrey Mwambe akitoa mada.

Kamati hizo ni Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma na Kamati ya Katiba na Sheria. 

Lengo la elimu hiyo ilikuwa ni kuwajengea Wabunge uelewa mpana wa masuala ya uwekezaji ambapo walipata fursa ya kufahamu kiundani majukumu ya TIC, namna Kituo kinavyovutia uwekezaji kwa kuzingatia hitaji la mwekezaji, sababu za kuwekeza Tanzania, vigezo vya mwekezaji kujisajili na TIC, vivutio vya uwekezaji na namna ambavyo vinachangia kuvutia uwekezaji mpya.

Pia umuhimu wa uwepo wa dirisha la huduma za mahala pamoja TIC  kwa wawekezaji na namna linavyofanikisha uwekezaji, faida za uwekezaji, nafasi ya Tanzania katika masuala ya uwekezaji, mgawanyo wa miradi ya uwekezaji kimkoa, namna ambavyo miundombinu mizuri inavyochangia kuvutia uwekezaji, na namna ambavyo uharaka wa upatikanaji wa idhini (vibali, vyeti na leseni) mbalimbali za kufanikisha uwekezaji zinavyovutia uwekezaji.

Vilevile Bw. Mwambe aliweka bayana namna ambavyo mataifa yote duniani yanavyoshindana katika kuvutia uwekezaji, changamoto za uwekezaji na mapendekezo ya maboresho ya  mazingira ya uwekezaji nchini ili kuvutia uwekezaji zaidi.

Naye Mhe. Dkt. Chegeni (Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma) amezungumza kuwa, kupitia semina wameweza kupata picha kubwa ya mwenendo na nafasi ya Tanzania kiuwekezaji duniani, Afrika na Afrika Mashariki.

'Tayari kuna mikakati na jitihada zinazochukuliwa na Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji lakini tuongeze kasi ili kufanikisha uwekezaji zaidi. Semina imechangia kuwaobgezea elimu zaidi ya masuala ya uwekezaji na kwamba watakuwa katika nafasi nzuri ya kuchangia pale hoja za masuala ya uwekezaji zitakapowasilishwa Bungeni', alisema.

Aidha Mhe. Chegeni alihimiza TIC iendelee kutoa elimu ya uwekezaji kwa wadau wote wakieleza TIC na majukumu yake, faida za uwekezaji kwa nchi na faida za mwekezaji akijisajili na TIC katika kufanikisha uwekezaji wake.