
Mwanasheria na Wakili wa kujitegemea kutoka Kampuni Mawakili CRAX LAW PARTNERS, Majura Magafu amesema viongozi na wabunge ni lazima wazingatie kanuni na sheria za haki za binadamu katika uwasilishaji wa michango yao bungeni.
Wakili Magafu ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na East Africa Television kuhusu tukio hivi karibuni katika kikao cha Bunge mjini Dodoma lakutumika kwa lugha ambayo imewakera baadhi ya wabunge wanawake na kusababisha wabunge wanawake wa Ukawa kutoka nje ya bunge.
Amesema kitendo hicho kimewagusa wanawake wote nchini na wanaume pia kwa sababu kazi ya ubunge ni sawasawa na kazi zingine na kwa misingi ya sheria za nchi matusi na lugha za kejeli haziruhusiwi ndani ya nchi kulingana na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano ambayo ndio Katiba Mama inazungumzia kuhusu namna yakuheshimu haki na utu wa kila mtu bila ubaguzi.
Amemtaka kiongozi wa shughuli za Bunge ambaye ni Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumwajibisha na kuchukua hatua stahiki kwa aliyehusika na udhalilishaji.
Kwa upande mwingine amewaasa wabunge ambao wanampango wa kugomea vikao vya Bunge waache ili wawakilishe na kujadili matatizo ya watanzania. Pia amewashauri wabunge wasivuruge sheria kwakutegemea watalindwa na kinga ya sheria za Bunge kwani zinamipaka katika utekelezaji wa haki za binadamu.