Jumatatu , 5th Sep , 2016

Wadau na watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam wameiomba serikali kufuatilia kiini cha kushuka kwa uingiaji wa meli za mizigo katika bandari hiyo.

Moja kati ya mabehewa 50 ya kubebe makasha, likishushwa kutoka kwenye meli, bandarini jijini Dar es Salaam.

Wametoa wito huo ili kujiridhisha iwapo madai ya kwamba kuwepo kwa tozo zisizo na ulazima ndiyo linalosababisha wafanyabiashara wengi sasa kutumia bandari nyingine za nchi jirani.

Ombi hilo limetolewa jijini Dar es Salaam wakati Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilipokutana na wadau hao ili kutaka kufahamu sababu za kupungua kwa meli za mizigo katika bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuchukua hatua za haraka za kurekebisha tatizo hilo.

Katika maelezo yao wadau hao wameiambia kamati hiyo ya bunge kwamba kinachoelezwa juu ya ukusanyaji wa mapato katika bandari ya Dar es Salaam kimekuwa si cha kweli kwani kwa sasa meli zinazotumia bandari ya Dar es Salaam katika kushuka na kupakia mizigo ni chache na nyingi kati ya hizo kwa sasa zinatumia bandari za nchi jirani.