Jumapili , 26th Mei , 2019

Serikali imewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na wa Halmashauri kuhakikisha kuwa ndani ya wiki mbili kuanzia sasa wawe wamekwishanunua vitambaa vigumu vya mpira ambavyo hutumika kuyafunika magodoro yanayotumiwa na wagonjwa.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt Dorothy Gwajima

Agizo hilo limetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt Dorothy Gwajima wakati alipofanya ziara kutembelea  hospitali ya Vijibweni iliyopo eneo la Kigamboni  jijini Dar es salaam.

Amesema anatoa siku 14 kuanzia sasa kwa waganga wakuu wa mikoa na halmashauri kuhakikisha kuwa magodoro yaliyopo kwenye Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati kwenye mikoa yao yanashonwa na kuwekea mifuko maalum ya mpira ili kuyafanya yarudi katika ubora wake. 

Watendaji wengine wamekuwa wakidai kuwa MSD wametuuzia magodoro haya siku nyingi na kitambaa chake laini hivyo yameanza kuchoka wakati inawezekana kununua kitambaa cha mpira, kwenye maduka yaliyopo yanayouza vitambaa vya mpira, mafundi wapo na kwa kuwatumia mafundi wenyeji wakashona magodoro haya yakarudi kuwa  mapya”, amesema.

Dkt Gwajima ameongeza kuwa hakuna sababu kwa watendaji hao kutumia visingizio vyao kwani bei ya kununulia mita kadhaa za vitambaa vigumu vya mpira  na za mashono ni ndogo na ni gharama zilizo ndani ya uwezo wa vituo vyetu vya kutolea huduma za afya.

Wakati huo huo, Dkt Gwajima amesifu hatua ya uongozi wa hospitali ya Vijibweni iliyopo wilayani Kigamboni kwa kuamua kukopa mashine ya Xray kutoka MSD ili waweze kuwahudumia wananchi walio wengi.

Tunazo hospitali zetu nyingi ambazo zinasubiri mgao wa serikali, hii haiwezekani, tunachosema ni kwamba kila hospitali itasimama yenyewe kupitia timu yake ya usimamizi huduma za afya ya halmashauri kwa kupanua wigo wa huduma  na kuvutia wateja wengi zaidi kutumia huduma hizo badala ya kuzifuata mbali na makazi yao kwa gharama kubwa,” amesisitiza Dkt Gwajima.

Akizungumzia kuhusu kuwepo kwa misongamano ya  wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, Dkt Gwajima amesema pamoja na ukweli kuwa baadhi ya maeneo kumekuwa na upungufu wa watumishi, yapo baadhi ya maeneo ambayo upungufu huo unachangiwa na uzembe wa baadhi ya watoa huduma katika kuwajibika.

Baadhi ya wataalam huwa wanachelewa kufika kazini na wakifika wanaishia kuona idadi ndogo ya wateja chini ya kiwango cha walau wateja 30 hadi 40 kwa siku kilichopo kwenye miongozo,” amesisitiza Dkt Gwajima.

Naibu Katibu Mkuu yupo katika ziara ya kikazi kutembelea mikoa ya Dar es salaam na Pwani ambapo kabla ya hapo alitembelea mikoa ya Morogoro, Dodoma, Njombe, Ruvuma, Iringa na Manyara.