Jumatatu , 1st Feb , 2021

Wananchi waishio Kata ya Pugu Stesheni Mtaa wa Kisiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Jijini Dar es salaam ,wameiomba Serikali kuingilia kati suala lao ili waweze kulipwa Fidia zao na Shirika la Reli Tanzania ,baada ya kupitiwa na Mradi wa Treni ya Kisasa ya SGR.

Baadhi ya maeneo ya wakazi wa Kata ya Pugu Stesheni Mtaa wa Kisiwani

Wakizungumza na EATV Saa Moja ,Wananchi hao wamesema kuwa kwa sasa wanaishi katika Mazingira magumu, baada ya kukatiwa huduma zote za Kijamii kama Maji lakini pia kufungwa kwa Njia walizokuwa wakitumia kupita ,ambapo inawalazimu kupita chini ya Makaravati yaliyoko chini ya Reli.

“Sisi kutokana na uhaba wa njia tunapita chini ya makalavati kwenda upande wa pili kwa ajili ya kufata mahitaji yetu ya kijamii, ambapo kwenye makalavati hayo maji yanapita hapohapo na maji hayo ni machafu na makalavati yenyewe sio rafiki na viongozi wanasisitiza tupite hapa ila juu tusipite” amesema mkazi wa ,Pugu stesheni Abdallah Juma

Wakizungumzia suala la Maji  wamesema kwa sasa wanalazimika kutumia Maji ya Visima walivyovichimba wenyewe, ambavyo kwa Ujumla hakuna Usalama wa Maji wanayoyatumia huku wakiliomba Shirika la Reli Tanzania kwenda kufyeka Vichaka vilivyopo katika Makazi yao kwa sababu Uhalifu umekithiri kwa sasa .

Bwana  Isaka Mawazo anasema tathmini walikwisha fanyiwa kilichosalia ni kulipwa tu Fidia ambapo mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ,Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa aliwaahidi Wananchi hao kuwa ndani ya Mwezi Mmoja na Nusu wangeshalipwa Fidia na kuondolewa katika Makazi hayo ili kupisha Mradi huo wa Treni ya SGR.

Jitihada za kumpata Mkurugenzi wa Shirika la Reli Masanja Kadogosa hazikufanikiwa lakini EATV SAA Moja ikamtafuta Mbunge wa Jimbo la Ukonga  Mhe. Jerry Silaa alieahidi kulitafutia ufumbuzi suala hili.