Ijumaa , 9th Jan , 2015

Wakulima Kilombero walalamikia kupata hasara ya zaidi ya tani laki 4 za miwa kubaki mashambani kutokana na kuingizwa sukari toka nje

Mashamba ya Miwa wilayani Kilombero

Wakulima wa miwa Kilombero mkoani Morogoro wameilalamikia  serikali   kushindwa  kudhibiti hujuma zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiashara  kuingiza sukari  kinyemela nchini bila kulipa kodi  na kuiweka katika  vifungashio vyenye lebo ya Kilombero na kusababisha zaidi ya  Tani laki  nne za miwa kubaki mashambani  bila kuvunwa  kutokana na viwanda  kushindwa  kuuza sukari  iliobaki viwandani .

Wakulima hao wametoa malamiko hayo mbele ya  kamati ya bunge ya kudumu  hesabu za serikali wakati walipotembelea kiwanda cha sukari Kilombero, ambapo wakizungumza kwa uchungu huku wakiwa wameshikilia mifuko ya sukari iliyotoka nchini Uganda na kufungwa upya katika mifuko ya Kilombero wakulima hao wamesema  wanapata hasara  kwa miwa kuendelea kubaki mashambani na kuomba kamati hiyo iwasaidie  kufikisha bungeni malalamiko yao .

Akijibu malalamiko ya wakulima hao mweyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge hesabu za serikali Zitto Kabwe amesema kamati inasubiri  taarifa ya TRA kuhusu uingizaji wa sukari nchini  kwa  kukwepa kodi   na mapendekezo ya  kamati ni kushauri bunge ili  bodi ya sukari iongezewe jukumu la usimamizi  kati ya  wazalishaji wa sukari na wakulima  ili kuhakikisha wakulima wanalipwa   kile wanchostahili badala ya wawezekezaji  kujinufaisha kupitia migongo ya wakulima.

Nao wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge hesabu za serikai  baada ya kusikiliza malalamiko ya wakulima juu ya miwa kubaki mashambani wameshauri wawekezaji wapanue viwanda au kuongeza viwanda vidogo.

Naye mkurugenzi wa bodi ya sukari Henry Semwaza amesema   wanahitaji bilioni 11 kulipa fidia wananchi 1554  ili kupisha  uwekezaji wa kiwanda kikubwa cha sukari   utakafanyka bonde la  Ruhipa wilayani Kilombero, yenye ukubwa wa hekta elfu 14  ambao utapunguza tatizo la  upungufu wa sukari  nchini.