Jumatatu , 28th Mar , 2016

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Seleman Liwowa awashauri wakulima na wafugaji kwa kushirikiana na kamati za Ardhi za vijiji katika wilaya hiyo kutenga maeneo kwa ajili ya Upandaji miti kwa lengo la kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Mkuu wa wilaya ya Kilindi Seleman Liwowa

Akizungumzia uvamizi wa maeneo ya mazingira asilia wilayani humo Liwowa, amesema serikali imeamua kuanzisha zoezi hilo ikiwa ni jitihada za kukabiliana na kupotea kwa uoto wa asili na kuwataka wananchi kuboresha aina ya kilimo kinachoweza kurejesha uoto.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa bado wanaendelea kuwaelimisha wananchi kutambua umuhimu wa misitu ambayo ipo katika hifadhi ili waweze kuilinda na kuitunza kwa ajili ya manufaa ya vizazi vijavyo.

Kwa upande wake Meneja wa wakala wa Huduma za Msitu katika wilaya hiyo Bw. Peter Fitwangile pamoja na aifsa misitu Rashid Kahungo wamesema suala la uhifadhi wa mazingira asilia linahitaji kila mwana jamii kushiriki hasa ulinzi wa misitu inayopakana na makazi ya watu.