Jumanne , 8th Dec , 2015

Kufuatia agizo alilolitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwa maadhimisho ya sherehe za uhuru tarehe 09 Desemba, 2015 zifanyike kwa kufanya usafi nchi nzima ili kuondokana na hali ya uchafu unaosababisha magonjwa.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Bw. Jumanne Sagini

Katibu mkuu ofisi ya waziri Mkuu TAMISEMI Jumanne Sigini ametoa tamko mbele ya waandishi wa habari mkoani Tanga kuhusu utekelezaji wa maelekezo ya Mh. Rais John Magufuli na kusema kuwa wakuu wa mikoa wanatakiwa kuhakikisha kuwa sera, sheria na kanuni mbalimbali za afya zilizopo zinasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo katika halmashauri zote ili kuzuia magonjwa ya mlipuko ikiwa ni pamoja na kipindupindu.

Aidha katibu mkuu amesema kuwa katika kufanikisha zoezi hilo halmashauri zinatakiwa kufanya maandalizi ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau mbalimbali na viongozi wakiwemo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, viongozi wa ngazi zote za TAMISEMI yaani halmashauri, tarafa, kata, vijiji, mtaa, vitongoji na wananchi wote wanashiriki kikamilifu ifikapo tarehe 09/12/2015 kuanzia saa 1:00 asubuhi mpaka saa 7:00 mchana.

Sambamba na hayo ameongeza kuwa halmashauri zinatakiwa kuandaa mikakati ya kudumu na kufanya usafi kuwa moja ya kipaumbele cha juu na kutoa taarifa Serikalini kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa angalau mara mbili kila mwezi kuanzia tarehe 15 Desemba,2015.

Pia ameeleza maeneo ambayo yanatakiwa kupewa kipaumbele kusafishwa kuwa ni pamoja na masoko, stendi, maeneo ya kuuzia vyakula, mifereji ya maji safi na maji taka, gereji, maeneo ya biashara, maeneo ya makazi, vyuo, shule, hospitali, vituo vya afya na zahanati.