
Waziri wa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa
Akitoa taarifa kuhusu uboreshaji wa huduma kwa walimu Jijini Dodoma Waziri wa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amesema ni Marufuku kuwaacha walimu kupita kila ofisi ya Halmashauri kutafuta huduma huku akisisitiza wasimamizi wanaotoa huduma kwa walimu kutimiza wajibu wao na kutokubweteka kukaa maofisini.
“ninawaelekeza Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya Wahakikishe Wanawasimamia watendaji wanaotoa huduma kwa walimu (Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM), Maafisaelimu, Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Wathibiti Ubora wa Shule), watendaji hawa niliowataja hakikisheni mnawafuata walimu shuleni, na kutatua kero na malalamiko yao kwa wakati.
Marufuku kuwaacha walimu kupita kila ofisi ya Halmashauri kutafuta huduma. Narudia tena mwalimu apelekewe huduma shuleni badala ya watoa huduma kukaa ofisini. Pia Mwalimu akiandika barua kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhitaji huduma, anapaswa kujibiwa kwa maandishi ndani ya siku 7 baada ya kupokelewa” amesisitiza