Alhamisi , 26th Nov , 2020

Aliyekuwa mtia nia wa Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Leonard Manyama ameelezea mtazamo wake juu ya wabunge 19 walioapishwa jijini Dodoma wa chama hicho bila idhini ya chama kuwa ni usaliti.

Aliyekuwa mtia nia Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Leonard Manyama

Akizungumza katika kipindi cha Supa breakfast, cha East Africa Radio, Manyama amesema ni matarajio yake kuwa wabunge hao watashikilia msimamo wao kuwa ni wabunge halali ilihali hawajatumwa na chama wala kanuni na miongozi ya chama kuzingatiwa.

“Kinachotokea kinataka kukatisha watu tamaa hakina hatma nzuri kwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, kilichofanyika ni usaliti kwa chama nadhani katibu anapaswa akatazama kwa maslahi mapana ya chama, wanachama na taifa kwa ujumla "amesema Manyama

Aidha kufuatia hayo yaliyojiri Manyama amewashauri viongozi wa chama chake kuchukua hatua juu ya wabunge hao kwani wengi wao wana nyadhifa mbalimbali ndani ya chama kitaifa.

“Kitu kinachotakiwa kifanyike ukiangali wengine ni viongozi wa chama kitaifa, wajumbe kwa maslahi ya nchi, chama, na taifa kiujumla  ningeshauri viongozi wa chama wawaache waendelee na hicho walichokiona kinafaa lakini wanaweza kuwavua nyadhifa zao zote kwenye chama, ili kujenga uaminifu kwenye chama” amesema Manyama

Kwa upande wake Dkt. Mayrose Majinge ambaye pia alikuwa mtia nia wa nafasi ya urais katika chama hicho amesema kuwa hawezi kusema lolote kuhusiana na suala hilo  mpaka awe amejiridhisha kwa kuwa na maelezo na data za kutosha huku akiamini ni mapema mno kuzungumza suala liliotokea.