Alhamisi , 10th Jan , 2019

Zaidi ya wanafuzi wapatao 500 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari Namikupa, Naputa na Tandahimba mkoani Mtwara hawajaripoti shuleni na kuleta sintofahamu kubwa miongoni mwa wadau wa elimu.

Wanafunzi

Kati ya wanafunzi 516 waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari katika shule hizo, ni wanafunzi 10 pekee ndio walioripoti shuleni mpaka sasa.

Akielezea juu ya kitendo hicho, Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Sebastian Waryuba amewaagiza Watendaji wa Kata kuwatafuta wanafunzi hao na kuwapeleka shuleni huku akiwataka wazazi kuacha visingizio vya kutolipwa fedha zao kutowapeleka watoto wao shuleni.

"Tukiendekeza vitu kama hivi, jamii yetu itazidi kuwa duni na itadidimia kabisa, wazazi wanataka kupata kisingizio fukani, eti kwasababu hatujalipwa fedha za korosho wakati mheshimiwa Rais ametoa elimu bure", amesema Mkuu huyo wa Wilaya.

Shule ya sekondari ya Namikupe imewasajili wanafunzi 219 ambapo mpaka sasa ni mwanafunzi mmoja pekee ameripoti katika shule hiyo, huku shule ya Naputa wakiripoti wanafunzi 5 kati ya 137 na shule ya Tandahimba wameripoti wanafunzi 4 kati ya wanafunzi 160.