Jumatatu , 15th Dec , 2014

Usalama wa watetezi wa haki za binadamu huko Loliondo nchini Tanzania, upo hatarini kutokana na mfululizo wa vitisho wanavyotumiwa watetezi hao, kutoka kwa watu wanaodhaniwa kuwa ni wale wanaoendesha kampeni ya kutaka kuchukua ardhi zaid ya wafugaji.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania - THRDC, Onesmo Olengurumwa (kulia), akiwa kwenye moja ya mafunzo ya kuwanjengea wanahabari uelewa kuhusu mazingira hatarishi katika kazi yao.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Bw. Onesmo Olengurumwa, amesema hayo leo na kwamba vitisho hivyo ni muendelezo wa kampeni ya muda mrefu ya kutaka kunyamazisha sauti za makundi ya watu uchukuaji wa ardhi ya eneo hilo pasipo kuangalia maslahi ya wakazi wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa Olengurumwa, hali imezidi kuwa mbaya hivi sasa kwani licha ya kupata vitisho hivyo, watetezi hao pia wamekuwa wakizushiwa kuwa sio raia wa Tanzania na kwamba wao ni vibaraka wanaopokea fedha kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kutekeleza mipango miovu.

Olengurumwa pia ameongeza kuwa kuongezeka kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kunakofanywa na vyombo vya dola kunachangiwa na kukosekana kwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti pamoja na bodi ya Wakurugenzi ya Tume ya Binadamu na Utawala Bora.

Kwa mujibu wa Olengurumwa, kwa takribani mwaka mmoja sasa serikali imeshindwa kuteua viongozi hao na kwa maana hiyo imekosa chombo huru ambacho ni kama kioo kwa serikali hasa linapokuja suala la utekelezaji na ufuatiliaji wa masuala yanayohusu haki za msingi za binadamu.

Ameongeza kuwa hata yanayotokea Loliondo hivi sasa kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na kutokuwepo kwa uongozi wa tume hiyo ambayo mara kadhaa imeonesha umahiri na uwazi mkubwa katika kushughulikia kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu zilizofanywa na vyombo vya dola.