Mradi wa Maji Meatu
Meneja wa RUWASA Mkoa huu wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala, ameviagiza vyombo vya watoa huduma ya maji kuhakikisha ndoo moja kwa miradi yote ya RUWASA inayotumia nishati ya jua, inauzwa Sh 30.
Majala ametoa maelekezo hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda, aliyezuru Wilaya ya Meatu kuzindua miradi ya maji.
"RUWASA kwa ujumla imeandaa mwongozo kuhusu bei za watumiaji maji katika maeneo yote nchini, ambapo tangazo lake la Serikali limetoka tarehe 5 Mwezi wa nane (2022), kwa hiyo, bei zile tayari zimeshaanza kutumika kwa hiyo naomba sana tusije tukawaumiza wananchi."- Amesema Meneja RUWASA Simiyu, Mariam Majala
Akizungumza muda mfupi baada ya kuzindua mradi wa maji ulioko Kijiji cha Mwaukoli wilayani hapo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda, amewataka kulindwa miradi ya maendeleo inayojengwa na serikali, kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.
"Maji yamekuwa mkombozi mkubwa sana kwa wananchi. Nani kama mama Samia (Rais). Kwa hiyo kazi yenu ni moja tu ambayo Mhe Rais ameniagiza kwenu, jambo kubwa kabisa aliloniagiza ni kutunza miundombinu hii ya maji. Kuhakikisha miradi hii yote ya maji na miradi mingine ya Serikali mnaitunza ili mwisho wa siku isaidie kizazi cha Leo na kesho zaidi," - amesema Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda.

