
Kauli hiyo ya wakazi wa mansipaa ya Bukoba, wameitoa baada ya serikali kukabidhi eneo la mradi kwa mkandarasi ambaye ni kampuni ya Kajuna Investment, kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo kipya cha mabasi, katika eneo la Kyakailabwa katika kata ya Nyanga, ambacho kilikwishawekewa miundombinu ya awali kwa gharama za zaidi ya shilingi milioni 500.
"Stand hii ina matatizo mengi, tuache la mvua kunyesha matope yakajaa, lakini pia haina jengo la abiria wakifika na mabasi ya usiku mfano yanayotoka Arusha hawana pa kupumzikia, haina uzio usalama ni mdogo na ni finyu" wamesema watumiaji wa kituo cha sasa.
"Katika mwaka wa fedha 2022/2023, halmashauri inatarajia kutekeleza mradi wa thamani ya shilingi milioni 999.9 kwa muda wa siku 150, shughuli zitakazofanyika ni ujenzi wa eneo la maegesho ya mabasi 26 kwa wakati mmoja, ujenzi wa mabanda tisa ya kusubiria abiria, uwekaji wa taa tano za mionzi ya jua na ujenzi wa mitalo" amesema Philbert Gozbert Mkuu wa Idara ya Viwanda, Bishara na Uwekezaji Manispaa ya Bukoba.
Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mradi wa kituo kipya cha mabasi katika eneo la Kyakailabwa ulifanyiwa usanifu na kuandaa mchoro na makisio ya gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 18.8, chini ya mradi wa uendelezaji wa miji, lakini manispaa hiyo haikuweza kupata fedha za utekelezaji wa mradi huo