Jumanne , 11th Mei , 2021

Wananchi wa kata za Kitendaguro na Bakoba ambao walijitolea nguvu zao kujenga barabara kwa lengo la kurahisisha mawasiliano katika kata hizo, wameilalamikia serikali kuharibu barabara yao baada ya kuanza ujenzi wa ukuta katika eneo yatakapojengwa makazi ya mkuu wa mkoa wa Kagera, na kwamba

Eneo ambalo unajengwa ukutwa

ujenzi wa ukuta huo utawafanya kukosa namna ya kutoka katika makazi yao.

Wakizungumzia suala hilo wananchi hao kutoka katika mitaa ya Kyamuhumula, Forodhani na Mtoni wamesema baadhi yao wamekaa katika mitaa hiyo kwa muda mrefu kutokana na kurithishwa maeneo hayo na wazazi wao, na kutumia fursa hiyo kuiomba serikali kulitafutia ufumbuzi wa haraka tatizo hilo.

Wenyeviti wa mitaa miwili kati ya mitatu yenye mgogoro, Audax Mathias wa mtaa wa Mtoni na Abela Nelson wa mtaa wa Kyamuhumula wamethibitisha kuwepo kwa mgogoro huo ambao asilimia kubwa unatokana na kuharibiwa kwa barabara ya kwenda katika makazi ya wananchi, huku wakieleza hatua ambazo zimechukuliwa.

Kwa upande wake afisa mipango miji wa manispaa ya Bukoba, Catress Rwegasira amesema kuwa wananchi wanaolalamika hawakuwepo katika eneo hilo lilipopimwa mwaka 1994 kwa ajili ya kujenga makazi ya mkuu wa mkoa.