Wanaochapisha uongo kuhusu ujumbe wa Kenya waonywa

Alhamisi , 30th Jul , 2020

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dkt Damas Ndumbaro, amewataka Watanzania kuisemea nchi mazuri ili kuwa na diplomasia nzuri na Mataifa mengine na kuachana na upotoshaji unaoenezwa mitandaoni hasa baada ya ujumbe wa Kenya uliokuwa ushiriki katika maziko ya Kitaifa kushindwa kufika.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dkt Damas Ndumbaro.

Dkt Ndumbaro ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam, kufuatia kuenea taarifa za uzushi katika mitandao ya kijamii, hususani baada ya ujumbe uliokuwa uiwakilishe Kenya katika hafla ya Kitaifa ya kuaga mwili wa Hayati Benjamin Mkapa, iliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru siku ya Julai 28, 2020, kushindwa kutua nchini kutokana na hitilafu za kiufundi.

"Ndege hiyo ya Kenya ilishindwa kutua Tanzania kutokana na hitilafu za kiufundi, ambazo ziligundulika na Rubani muda mfupi baada ya kuruka kutoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Nairobi, kwenye mitandao watu wanahusisha hilo na COVID-19 na mambo mengine" amesema Dkt Ndumbaro.

Aidha ameongeza kuwa, "Niwaambie Watanzania tuna muda mchache sana ambao tunapaswa kuutumia kufanya mambo ya maana na kimaendeleo siyo kukaa mitandaoni kusuka maneno ya uongo, fitina na ugombanishi, niwasihi Watanzania watumie vizuri muda wa mitandaoni kwa sababu wanayoyafanya ni uhalifu". 

Dkt Ndumbaro ameongeza kuwa kuandika au kuchapisha taarifa za uzushi na zisizo na uthibitisho ni kinyume cha sheria za mitandao ya mwaka 2015 na adhabu yake ni pamoja na kifungo gerezani.