Jumatano , 18th Aug , 2021

Jeshi la Polisi nchini Tanzania, kupitia Kikosi cha Polisi cha Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA), linawashikilia watu wanne, kwa tuhuma za kuiba vyuma vya miundombinu ya reli mkoani Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha TAZARA, SACP Mwamini Rwantale akionyesha vyuma vya miundombinu ya reli .

Kamanda wa Polisi Kikosi cha TAZARA, SACP Mwamini Rwantale, ametoa taarifa hiyo akizungumzia doria ya kudhibiti vitendo vya hujuma kwenye miundombinu ya reli ya shirika hilo, kuanzia Dar es Salaam, hadi Tunduma mkoani Songwe.

Amewataja waliokamatwa kufuatia tuhuma hizo ni, Bakari Mussa (54), mkazi wa Yombo, ambaye ni mfanyabiashara na Abraham Emmanuel (35), mlinzi na mkazi wa Buguruni. Wengine ni, fundi wa kuchomelea vyuma, Frank Jerome (32), mkazi wa Temeke na Waziri Alli (25), dereva wa pikipiki ‘Bodaboda’.

"Kupitia doria na misako, kikosi kimefanikwa kuwakamata  watu wanne  kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya reli. Walikamatwa watuhumiwa hao eneo la vertinaly Temeke,  wakiwa na vyuma mbalimbali vya miundombinu ya reli," amesema Kamanda Rwantale.
 
Kamanda Rwantale amesema Watuhuma wote watafikishwa mahakamani hivi karibuni kujibu tuhuma zinazowakabili.