
Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA, Esther Matiko
Swali hilo ameliuliza Bungeni leo Februari 2, 2021, katika Kikao cha kwanza cha mkutano wa pili wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kulielekeza kwa Wizara ya Elimu ambapo amesema kuwa Watanzania wengi wenye sifa za kuendelea na elimu ya chuo kikuu wamekuwa wakishindwa kuhimili gharama za makato.
"Watanzania wengi wenye sifa za kwenda vyuo vikuu wanatamani sana kupata mikopo, lakini mikopo hii ina riba kubwa sana ya asilimia 15 na penalty ya asilimia 6, wanufaika wengi wanashindwa kubeba huu mzigo. Je ni lini serikali italeta mabadiliko ya sheria hii walau tupeleke kwenye asilimia 8 ili tuwe na lengo la kutoa wajuzi na siyo kugeuzwa kama chanzo cha mapato", amehoji Esther Matiko
Akijibu swali hilo Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, amesema kuwa lengo la kuanzisha mfuko wa mkopo ilikuwa ni kuhakikisha watu wafanye marejesho ili mikopo ijiendeshe yenyewe na kuongeza idadi ya wanufaika na kusisitiza kwamba, wanaochukua mikopo walipe kwa wakati na wenye fedha warejeshe wasingoje kukatwa hizo asilimia 15.