Jumapili , 8th Mei , 2016

Serikali wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro imewataka wananchi kuunda vikundi shirikishi ili kusaidia kuondokana na migogoro inayoibuka baina ya wakulima na wafugaji kufuatia kudaiwa wafugaji kuruhusu mifugo yao kuingia katika mashamba ya wakulima.

Mkuu wa wilaya ya Mvomero Bi. Betty Mkwasa

Licha ya Serikali kuanza kuweka mpaka wa mfereji mkubwa wa kutenganisha eneo la wafugaji wa kijiji cha Kambala na wakulima wa bonde la Mgongola lakini bado uvunjifu wa amani umeendelea kujitokeza baada ya wafugaji kuamua kuvuka mpaka huo na kuvamia na kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.

Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Bi. Betty Mkwasa, wakulima hao wamesema wanasikitishwa na kitendo cha wafugaji hao kuvuka mpaka uliwekwa na serikali na chini ya uamuzi wa Mahakama, na kuiomba serikali kupeleka wanajeshi ambao watasaidia kutatua kero hiyo.

Bi. Betty Mkwasa, alilazimika kutumia usafiri wa trekta kwenda kujionea hali ilivyo kati ya wakulima na wafugaji na kushughudia vitendo vya uvunjifu wa amani baada ya ng’ombe kuingia katika mashamba ya wakulima ambapo amewataka wakulima kufuata sheria huku akiagiza kuundwa vikundi vya ulinzi na usalama kwa wakulima na wafugaji vitakavyo tambuliwa na serikali.