Ijumaa , 14th Oct , 2016

Taifa la Tanzania leo limeadhimisha miaka 17 tangu kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambapo maadhimisho ya kitaifa yamefanyika Mkoani Simiyu Wilaya ya Bariadi na kuongozwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.

Hayati Mwalimu Julius Nyerere

Maadhimisho hayo yaliambatana na kuzimwa kwa Mwenge wa Uhuru pamoja na kilele cha wiki ya vijana yakiwa na kauli mbiu isemayo Vijana ni nguvu kazi ya taifa, washirikishwe na wawezeshwe.

Wakati watanzania wakiadhimisha miaka 17 ya kifo cha Baba wa Taifa, Jijini Dar es Salaam wito umetolewa kwa viongozi mbalimbali kote nchini kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuwajali wananchi, kutenda haki bila ya ubaguzi na kuulinda Muungano wa Tanzania uliojengwa na waasisi wetu Mwalimu Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Ilala Mhe. Charles Kuyeko amesema ni lazima sasa viwanda vilivyoanzishwa na Mwalimu Nyerere vifufuliwe huku Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Ally Hapi akiwakumbusha viongozi kutekeleza azimio la Arusha ili kujenga uongozi unaojali utu na uzalendo.

Nao viongozi wa zamani wa chama cha TANU na baadaye CCM wamewaasa viongozi walio madarakani kuulinda Muungano pamoja na kuondoa pengo baina ya masikini na matajiri ili kuweka usawa kwa wananchi wote.

Aidha, katika kuadhimbisha kumbukumbo ya kifo cha Mwalimu Nyerere, vijana zaidi ya 300 na taasisi 10 kwa pamoja wameshiriki kufanya shuguli za kujitolea hasa ya mazingira ili kumuenzi Hayati Baba wa Taifa.