Jumapili , 20th Nov , 2022

Kutokana na kukithiri kwa migogoro ya wafugaji na wakulima mkoani Lindi, baadhi ya wenyeviti Serikali za vijiji, maofisa watendaji wa vijiji na kata wametajwa kuwa chanzo.

Akizungumza katika mkutano na wanavijiji, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Hashimu Komba aliwataka wafugaji walioingia na kuingiza mifugo yao kwa njia za panya kuondoka mara moja kurejea walikotoka kabla ya kuanza operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu.

Watendaji hao wamedaiwa kushiriki vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji wanaoingiza mifugo bila kufuata utaratibu.

Mmoja ya mkazi wa Ngumbu Liwale amesema mauaji yanayotokea, huchangiwa na baadhi ya viongozi wa vijiji na kata kukubali kupokea rushwa, kwa lengo la kuwaruhusu wafugaji wasiofuata taratibu kuingiza mifugo yao kupitia njia za mkato bila kufuata taratibu.

Mkoa wa Lindi ni kati ya mikoa iliyopokea wafungaji kutoka bonde la Ihefu, lakini baada ya kuingia kumetokea migogoro ya wafugaji na kusababisha mauaji kati ya wafugaji na wakulima katika wilaya za Kilwa, Liwale, Nachingwea na Ruangwa, ambapo hadi kufikia sasa watu wasiopungua 15 wamefariki.