Ijumaa , 23rd Feb , 2018

Watu watano akiwamo raia wa Burundi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama ya kufanya mauaji ya mwanaharakati wa kutetea wanyama pori Wyne Lotter.

Wakili wa Serikali Mwandamizi,Yamiko Mlekano amewataja washtakiwa hao kuwa ni raia wa Burundi, Nduimana Jonas maarufu Mchungaji mkazi wa Kamenge Burundi na mfanyabiashara Godfrey Salamba mkazi wa Kinondoni Msisiri A. Wengine ni mfanyabiashara Inocent Kimaro  mkazi wa Temeke Mikoroshini, mfanyabiashara Chambie Ally mkazi wa Kia/Boma na Ofisa wa NBC, Robert Mwaipyana mkazi wa Temeke Mikoroshini. 

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ambapo katika shtaka la kwanza wanadaiwa kuwa walikula njama ya kufanya mauaji ya Lotter. Na katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la mauaji ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 16, 2017 katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selasie Kinondoni Dar es Salaam kwa kumuua Lotter. 

Washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu lolote kutokana na mahakam hiyo kutokuwa na mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo ambayo pia imetajwa kuwa haina dhamana. 

Washtakiwa hao, Machi 6,2018 wataunganishwa na washtakiwa watatu waliokuwa wanakabiliwa na kesi hiyo awali ambapo kesi yao ipo katika hatua ya kutajwa kwa sababu upelelezi wake bado haujakamilika, akiwemo Meneja wa Benki ya Backlays, Khalid Mwinyi mkazi wa Mikocheni B, mfanyabiashara Rahma Almas mkazi wa Mbagala B na Mohammed Maganga (61) mchimba makaburi. 

Kesi imeahirishwa hadi Machi 6, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Wyne Lotter alikuwa Mkurugenzi na Mwanzilishi-Mwenza wa shirika lisilo la kiserikali la Palms Foundation ambalo linafanya shughuli zake nchini Tanzania kwa kupinga ujangili.