Jumapili , 17th Oct , 2021

Katika kuendelea kuhakikisha wananchi wanapata ajira za kudumu za zile za muda mfupi ili kujipatia kipato, serikali imeweka wazi kuwa kipaumbele cha ajira katika miradi ya ndani ni kwa wazawa wenye sifa.

Sehemu ya mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere

Hayo yameelezwa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa ya wiki, ambapo amesema katika mradi wa ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere asilimia 89 ya wafanyakazi ni watanzania.

''Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere una Wafanyakazi Watanzania 7,713 sawa na 89% ya wafanyakazi wote 8,635. Mpaka sasa Wakandarasi wameshalipwa Sh Trilioni 2.832 kati ya Trilioni 6. 558 zitakazotumika kugharamia ujenzi huu,”amesema Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa.

Kwa upande mwingine amesema serikali inaendelea kuifungua nchi kwa kuhakikisha barabara zote zinapitika na kuwawezesha watu kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila changamoto hata kama wapo vijijini iwe rahisi kufikia huduma maeneo ya mijini.

''Hadi Juni, 2021, TARURA imetumia Sh Trilioni 1. 297 kutengeneza KM 24,979 za barabara, KM 955.35 kwa kiwango cha lami, KM 16,857 kwa kiwango cha changarawe pia wamejenga madaraja 231 na makalvati mapya 1,325. Mwaka huu wa fedha, Serikali imeitengea TARURA Bilioni 934,” ameongeza Gerson Msigwa, Msemaji Mkuu wa Serikali.