Jumamosi , 8th Dec , 2018

Serikali imepiga marufuku usafarishaji wa Korosho nje ya nchi kwa mfanyabiashara yeyote ndani ya nchi badala yake imetoa ruhusa ya tani 2000 ambazo zilinunuliwa kabla ya serikali haijaamua kuingilia kati kununua zao hilo.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga

Agizo hilo la serikali limetolewa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb), leo Disemba 8, 2018 wakati akizungumza kwenye Mkutano wa wamiliki wa viwanda vya kubangua korosho kwenye ukumbi wa mikutano kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.

Waziri  Hasunga amesema wakati serikali inaendelea kukamilisha uhakiki wa wakulima wa Korosho pamoja na kuendelea na malipo ya wakulima mpaka hivi sasa wakulima 77,380 wamekwishalipwa hivyo hakuna korosho itakayoruhusiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi bila utaratibu maalum badala yake korosho zote zitabanguliwa nchini.

Hasunga aliongeza kuwa Korosho zitakazoruhusiwa kwenda nje ya nchi ni zile tani 2000 pekee zilizonunuliwa mnadani na kampuni mbili kwa utaratibu uliokuwa ukitumika awali.

Hakuna kampuni yoyote wala mfanyabiashara yoyote anayeruhusiwa kusafirisha korosho nje ya nchi baada ya tamko la serikali kutolewa” Alikaririwa Mh Hasunga.

Tuwe na uwezo wa kubangua ama hakuna lakini korosho zote zitabanguliwa nchini, hivyo wito wangu kwa wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya ubanguaji usiku na mchana” Alisema.

Hasunga aliongeza kuwa serikali imeanza mchakato wa kuwafuatilia baadhi ya wafanyabiashara wenye uwezo wa kujenga viwanda kwa kufunga mitambo ndani ya muda mfupi.