Waziri Kangi Lugola aionya CHADEMA

Ijumaa , 8th Nov , 2019

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amekionya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuhusiana na msimamo wake wa kujitoa kwenye zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa madai ya kwamba, anadhani mpango huo huenda ukawa na nia ya kuchafua amani.

Waziri Lugola, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza jijini Dodoma, ambapo amesema kama Serikali kupitia Jeshi la Polisi, wamejipanga kuhakikisha zoezi zima la uchaguzi linafanyika kwa amani na usalama.

"Nina taarifa kuwa chama kimoja kimejitoa kwenye Uchaguzi, ni imani yangu chama hicho kinaweza kuwa na mipango ya kuvuruga amani ya nchi hii, nitoe onyo hakutakuwa na nafasi ya chama cha siasa kuratibu mipango ya kuvuruga amani, Serikali tumejipanga kutumia nguvu hakuna amani inavurugwa" amesema Kangi Lugola.

Jana Novemba 07, 2019, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupitia Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, kilitangaza azimio la kutoshiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kile walichokidai kuna baadhi ya mambo hayako sawa.

Novemba 24, 2019, Wananchi wa Tanzania wanatarajiwa kushiriki zoezi la kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa.