Ijumaa , 23rd Feb , 2018

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ameuagiza uongozi wa wakala TFS kujenga kituo cha ulinzi wa kudumu katika eneo la chanzo cha maji ya mto Zigi kilichopo ndani ya Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani ili kulinda chanzo hicho.

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari  baada ya kutembelea eneo la chanzo hicho na kukuta uharibifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya wananchi wanaodaiwa kuchimba madini ya dhahabu katika eneo hilo la hifadhi ambapo ni kinyume cha sheria.

"Nimeagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania  (TFS) wajenge kituo cha ulinzi cha kudumu katika eneo hili, na waweke walinzi wetu wa kudumu hapa badala ya kutegemea kufanya patrol (doria) na kuondoka, kwa sababu eneo hili wananchi wanaamini lina madini ya dhahabu kwa hiyo kila siku wataendelea kuja kujaribu kuvuna dhahabu kutoka hapa", amesema Dkt. Kigwangalla.

Pamoja na hayo, Dkt. Kigwangalla ameendelea kwa kusema "kwa sababu sisi kazi yetu ni kuhifadhi maliasili ambayo tumepata kama urithi wa nchi yetu, niwahakikishie kwamba tutaimarisha ulinzi kwa kuanzisha kituo cha ulinzi hapa ili askari wawe wanabadilishana na kudhibiti kabisa uharibu ambao umekuwa ukifanyika, kwa sababu maji yanayotoka katika chanzo hiki yanakwenda kunywesha Muheza yenyewe na wilaya wa Tanga, tukiharibu hapa yatakosekana maji safi na salama".

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala huyo, Prof. Dos Santos Silayo amesema pamoja na eneo hilo kwa sasa kuwa linalindwa na askari wa Suma JKT watahakikisha ulinzi unakuwepo muda wote kwa kutekeleza agizo hilo la Waziri la kujenga kituo cha ulinzi cha kudumu ili askari wawepo katika eneo hilo muda wote.