Jumanne , 13th Apr , 2021

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa amesema serikali itahakikisha sekta binafsi inashamiri kwa kuainisha fursa zilizopo na kuweka vipaumbele vitakavyowezesha maendeleo ya sekta hiyo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa

Mh. Majaliwa amesema hayo leo bungeni, akiwa anawasilisha bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu ambapo ameihakikishia sekta binafsi kuimarishwa kutokana na umuhimu wake katika ustawi wa kiuchumi na kijamii.

"Serikali kupitia Mpango wa Mwaka 2021/2022 itaendelea kuhakikisha kuwa sekta binafsi inashamiri kwa kuainisha fursa zilizopo, kuweka vipaumbele vitakavyowezesha maendeleo ya sekta binafsi na kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji," amesema Mh. Majaliwa.

Pia Waziri Mkuu Majaliwa ametoa rai kwa sekta binafsi kuleta mpango mahususi utakaounga mkono mipango ya serikali ikiwemo katika kutengeneza ajira.

"Nitoe rai kwamba sekta binafsi ilete mpango mahsusi kuhusu namna ambavyo itaunga mkono mipango na mikakati ya Serikali ikiwa ni pamoja na kutengeneza ajira milioni nane katika kipindi cha miaka mitano," amesema Mh. Majaliwa.