Jumamosi , 8th Aug , 2020

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi ihakikishe inaboresha utoaji wa elimu ya ufugaji bora kwa wafugaji ili kuiwezesha mifugo yao kuwa na ubora na uzito mkubwa badala ya mifugo ya aina hiyo kuonekana kwenye maonesho pekee.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu ambaye amemuwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika sherehe hizo ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Agosti 8, 2020) katika kilele cha Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nane Nane Kitaifa kwenye Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu. 

Mara nyingi ng’ombe wenye uzito wa kilo mia nane, mia tisa nawakuta kwenye maonesho tu lakini hatuwaoni kwa wafugaji. Hawa anawatunza nani na kwa nini tusiwaambie wawatunze kama mnavyowatunza. Lazima tuwe na ng’ombe wanaofugwa na wafugaji wenye uzito huo, hivyo wafundisheni namna ya kuwatunza”, amesema Majaliwa.

Ameongeza kuwa, “Nimetembelea baadhi ya mabanda kwenye viwanja hivi vya Nyakabindi na nimeona bidhaa nyingi zinazotokana na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, huu ni ushahidi tosha wa mchango wa sekta ya kilimo katika kufikia uchumi wa kati. Tukumbuke kwamba safari yetu ya kujenga uchumi wa viwanda inaendelea".

Amesema kupitia maonesho hayo ya 28 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993, wakulima, wafugaji, wavuvi, wanaushirika na wajasiriamali hupata fursa ya kuonesha na kujifunza matumizi ya teknolojia bora za kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji wa uhakika wa chakula sambamba na kukidhi mahitaji ya viwanda na masoko ya ndani na nje ya nchi. Kauli mbiu ya sherehe hizo kwa mwaka huu ni “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020”.