Jumanne , 11th Jun , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Rwanda waje wawekeze katika sekta mbalimbali na kwamba Serikali itawapa ushirikiano wa kutosha.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Juni 11, 2019 alipofanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Rwanda, Donatille Mukabalisa, Ofisini kwake Bungeni jijini Dodoma.

Amesema Serikali ipo tayari kuwapokea wawekezaji kutoka katika nchi hiyo ili waje kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, kilimo, madini na utalii.

Waziri Mkuu amesema Tanzania na Rwanda ni nchi zenye uhusiano mzuri, hivyo amemwakikishia Spika Donatille kwamba Serikali itauimarisha uhusiano huo.

Aidha Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambao utarajiwa kusaidia katika usafirishaji wa mizigo kwenda hadi nchini Rwanda.