Ijumaa , 4th Oct , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa siku tatu kwa Kaimu Mweka Hazina wa wilaya ya Itigi mkoani Singida, Optatus Likiliwike, kuhakikisha anarejesha kiasi cha Shilingi Milioni 1.6, fedha ambazo alijilipa kama posho kinyume cha utaratibu.

Agizo hilo amelitoa leo Oktoba 4, 2019, akiwa katika ziara yake ya siku nne mkoani Singida, ambapo amesema kuwa anataka athibitishe kurejeshwa kwa fedha hizo kwa macho yake mwenyewe, kabla ya ziara yake kuisha siku ya Oktoba 7.

Kabla sijamaliza ziara tarehe 7, nataka nione karatasi ya malipo ya benki 'pay in slip' kwahiyo adhabu yako kaweke fedha benki na niione hiyo 'pay in slip' kabla sijaondoka,wewe si ndiye Otto au Optatus?, Julai ulilipwa posho ya safari ili uende Dodoma kukamilisha mahesabu ya bajeti, lakini hukwenda na taratibu za fedha zinasema ukitumia fedha, urejeshe, wewe ulifanyaje?" amesema Waziri Mkuu.

Akitolea ufafanuzi wa fedha hizo, ambazo alitengewa ili aende Dodoma kwa ajili ya kukamilisha mahesabu ya bajeti, Mweka hazina huyo alikiri kuzichukua fedha hizo na kwamba kutokana na majukumu mengi aliyonayo, alishindwa kwenda na badala yake akawa anaenda siku za mwisho wa juma kwa kile alichokidai kuwa si kazi zote zilikuwa zikimtaka kwenda huko.

Aidha katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka afisa huyo, arejeshe kiasi cha Shilingi milioni 196 za ujenzi wa ofisi ya Halmashauri, ambazo zimetumika kinyume na zilivyopangwa.