Jumanne , 14th Mei , 2019

Waziri mkuu Kassim Majaliwa, amewasimamisha kazi Wakurugenzi saba wa Tume ya Umwagiliaji, akiwemo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo leo, Jumanne, Mei 14, 2019, wakati wa kikao na viongozi wa tume hiyo kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Mawaziri, Manaibu Waziri na Makatibu Wakuu.

“CAG afanye haraka uchunguzi wa kina, tunataka kujua ni nani alikuwa mlango wa ubadhirifu huu. Hatutamuonea mtu, wote watakaothibitika kuhusika na matumizi mabaya ya fedha watachukuliwa hatua.”

Mbali na kuwasimamisha kazi wakurugenzi hao, pia Waziri Mkuu ameagiza watumishi wengine 21 wa tume hiyo wachukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na utendaji usioridhisha kwenye miradi mbalimbali inayosimamiwa na tume hiyo.

Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua hiyo kutokana na udhaifu wa kiutendaji ndani ya tume hiyo ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za miradi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, upendeleo na kukosa umakini.

“Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya ubadhirifu uliofanyika katika miradi ya umwagiliaji.” ameongeza.