Jumapili , 20th Aug , 2017

Wananchi wameagizwa kufuata utaratibu wa sera unaotaka wananchi kupata matibabu katika hospitali za Rufaa ni lazima awe ameandikiwa rufaa na siyo kila mtu aende moja kwa moja kwenye hospitali hizo.

Waziri Ummy akiwa na mgonjwa katika kituo cha Afya cha ya Mazwi kilichopo Manispaa ya Sumbawanga

Hayo yamezungumzwa leo na  Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akiongea na watumishi wa sekta ya afya wa Mkoa na Wilaya mkoani Rukwa ambapo ameagiza Manispaa ya Sumbawanga kuongeza kujenga vituo vya afya ili hospitali ya Rufaa ya mkoa ibaki kutoa huduma za kibingwa .

"Serikali inaboresha hospitali za Rufaa za Mkoa kwa ajili ya huduma za kibingwa hivyo hospitali hizo ziweze kutoa huduma za kimatibabu ya kibingwa kwa watu wenye uhitaji huo," alisema

Waziri Ummy akizungumza na Wagonjwa juu ya huduma

Pamoja na hayo Waziri Ummy amesema kulingana na kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini ni vyema na mkoa kujenga vituo vitakavyoweza kutoa huduma kwa wananchi waliopo maeneo husika kuliko kujenga hospitali ya Wilaya ambayo wananchi waliopo maeneo ya mbali wapate huduma za afya huko huko karibu na huduma hizo ziwe bora.

“Fanyeni maamuzi yenye manufaa kwa wananchi wa wilaya yenu ili muwasogezee huduma watu wenu, kwa Wilaya ya Nkasi  mnatakiwa kujenga hospitali ya wilaya ya serikali ambapo Wizara itawasaidia kutoa milioni 350 kati ya 650 ambazo zitajenga wodi ya wazazi, maabara pamoja na nyumba moja ya mtumishi" aliongeza.